Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Nouri Hamedani, katika kikao chake na washiriki wa hafla ya kuusindikiza na kuuzika mwili mtukufu wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, huku akirejelea nafasi ya juu na adhimu ya shahidi huyo, alisema:
Huenda hata leo bado watu wengi hawajatambua ipasavyo ni shakhsia ya kiwango gani na kubwa kiasi gani ambayo tumempoteza. Mimi nilimfahamu tangu miaka ya thelathini (Hijria Shamsia), na maisha yake yote yalijaa mambo muhimu, yenye thamani kubwa na yanayostahili kuzingatiwa.
Ayatullah huyo aliendelea kwa kurejelea ushiriki mkubwa wa wananchi katika hafla za kuaga na kuusindikiza mwili wa Kiongozi Shahidi wa Iran ya Kiislamu, akasema: Katika siku hizi chache zilizopita, dunia nzima ilibaki katika mshangao kutokana na ukubwa wa mahudhurio ya wananchi, na Inshaallah katika siku zijazo ushiriki huu utakuwa mkubwa zaidi.
Marjii huyu wa Taqlid aliendelea kusisitiza: Maadui wafahamu kwamba mahudhurio haya ya kishujaa yanaonesha sehemu ndogo tu ya wale waliokuwa wakimpenda na kumheshimu. Mtu huyu wa Mwenyezi Mungu ana wapenzi na wafuasi wengi sana duniani kote, wote wanapaswa kutambua kwamba mgogoro wetu ni dhidi ya fikra za ubeberu, dhulma na uhalifu unaofanywa na madola ya kibeberu, yaani Marekani na utawala wa Kizayuni. Taifa hili halitakubali kamwe kudhulumiwa, kwani utamaduni wetu wa kidini hauturuhusu kushirikiana na madhalimu wala ubeberu.
Akiwalaani wahusika wa uhalifu huu, alisisitiza: Wahusika wa jinai hii wafahamu kwamba kulipiziwa kisasi ni jambo la hakika na lisiloepukika.
Ayatullah Nouri Hamedani, mwishoni mwa hotuba yake, akiwausia viongozi wa nchi alisema: Viongozi waithamini neema ya wananchi hawa, na kwa kuhifadhi umoja na mshikamano wajitahidi kutatua matatizo ya nchi. Pia walinde na wahifadhi nguzo imara ya Wilayat al-Faqih. Ninaamini kwamba lengo kuu na la kwanza la maadui ni kudhoofisha nafasi hii, na ninatoa onyo kwa wote, hususan watu wenye ushawishi na viongozi wa nchi, walizingatie kwa uzito mkubwa suala hili.
Maoni yako